Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni kwa ajili ya mipango jumuishi na maendeleo endelevu ya nchi na yataongeza uwazi katika kugawa rasilimali zilizopo kuendana na uwiano wa idadi ya watu katika ngazi zote za utawala. Halikadhalika matokeo yatatumika na Serikali na wadau wengine katika kufuatilia na kutathmini mipango mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikijumuisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Dira ya Zanzibar 2050, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2021/22 - 2025/26 na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (2021/22 - 2025/26), Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050 na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063. Taarifa hizi zitaipima Tanzania katika hatua iliyofikia kwenye utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu; Mpango ambao unalenga kuleta usawa na kutokomeza umaskini wa aina zote ukiwemo umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030 kwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeachwa nyuma.
Idara ya Habari MAELEZO